26 Septemba 2020 - 11:17
Kiongozi wa Republican apingana na Trump, asisitiza madaraka yatakabidhiwa kwa njia ya amani

Kiongozi wa chama cha Republican katika Seneti ya Marekani Mitch McConnell ameungana na viongozi wengine wa chama hicho kutetea mfumo wa demokrasia ya kikatiba ya nchi hiyo na kupinga msimamo wa rais Donald Trump wa kukataa kukiri hadharani kwamba atakabidhi madaraka kwa amani baada ya uchaguzi wa urais utakaofanyika Novemba 3.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, McConnell amesema: "Mshindi wa uchaguzi wa Novemba 3 atatawazwa Januari 20. Kutakuwa na mapokezano ya amani, sawa kabisa na vile ambavyo imekuwa katika kila miaka minne tangu 1792."

Mbali na kiongozi huyo wa Warepublican katika Seneti, wabunge wengine kadhaa wa chama hicho wamejitokeza kuunga mkono kikamilifu makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani kufuatia matamshi ya siku ya Jumatano ya Trump.

Seneta Mitt Romney ameandika katika ukurasa wa Twitter: "Msingi wa demokrasia ni kukabidhi madaraka kwa njia ya amani...wazo lolote la kuonyesha kwamba kuna uwezekano wa rais kutoheshimu hakikisho hili la kikatiba, halitasawariki na wala halikubaliki."

Mnamo siku ya Jumatano Trump aliulizwa tena na mwandishi wa habari kuhusu utayarifu wake wa kukubali matokeo ya uchaguzi wa urais endapo atashindwa na kukabidhi madaraka kwa njia ya amani, lakini kwa mara nyingine alirudia tena jibu lake la kila mara kwamba: "Tunaendelea kuangalia nini kinatokea".

Trump amesisika akidai kwamba hatoshindwa katika uchaguzi wa Novemba isipokuwa kama Wademocrat watautumia upigaji kura kwa njia ya posta kufanya udanganyifu na uchakachuaji mkubwa. Kiongozi huyo anapinga utaratibu wa kupiga kura kwa njia ya posta ambao unaungwa mkono na Wademocrat na baadhi ya magavana wa majimbo ya nchi hiyo kwa ajili ya kuepusha maambukizi ya virusi vya corona endapo wapigakura wote watalazimika kupiga kura zao vituoni.

Msemaji wa Ikulu ya White House Kayleigh McEnany amewaambia maripota kwamba Trump "atakubali matokeo ya uchaguzi huru na wa haki."

Wakati tarehe ya uchaguzi wa rais wa Marekani inazidi kukaribia huku Trump akifanya juu chini ili asishindwe katika uchaguzi huo, hadi sasa maafisa kadhaa wa nchi hiyo wametahadharisha juu ya hatari na matokeo mabaya ya kutoshinda Trump katika kinyang'anyiro hicho.

Chunguzi za maoni zinaendelea kuonyesha kuwa Joe Biden mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democrat ana nafasi nzuri zaidi ya kuibuka mshindi katika uchaguzi huo.../

342/